Waziri wa ardhi Alice Wahome amewapa wakazi wa Mosiro, kaunti ndogo ya Narok Mashariki, kaunti ya Narok, hii ikiwa ni mojawepo wa hatua muhimu za kuwezesha jamii ya eneo hilo.
Hatimiliki hizo 1,348 zilitolewa kwa wakazi wa Oloosokon na kupiga jeki umiliki wa ardhi na usalama kwa jamii ya eneo hilo.
Wahome alisisitiza umuhimu wa umiliki wa ardhi kwa maendeleo ya wakazi na jamii kwa jumla.
Ardhi sio tu mali ya kiuchumi. Ni chanzo cha utambulisho, usalama na uthabiti wa watu wetu,” alisema Wahome.
Alisema hatua hiyo ya serikali ya kutoa hatimiliki za ardhi, ni ishara ya kujitolea kwake kuhakikisha kila mkenya anapata nafasi ya kumiliki haki.
Kulingana na waziri huyo, hafla hii inaashiri kujitolea kwa serikali kutatua changamoto za kihistoria za ardhi na kuimarisha haki ya umiliki wa ardhi.
Wahome alikuwa ameandamana na katibu katika wizara hiyo Nixon Korir, aliyesema serikali imejitolea kufanyia marekebisho mageuzi katika sekta ya ardhi ili kuharakisha ukuaji wa uchumi na udhabiti wa kijamii.
Kwa upande wake gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu, alishukuru serikali ya taifa kwa juhudi zake za kuunga mkono maendeleo ya kaunti ya Narok kupitia utoaji hatimiliki za ardhi.