Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kuwezesha ufadhili wa masomo katika kaunti zote 47 kupitia Hazina ya Kitaifa ya Kusimamia Shughuli za Serikali (NGAAF).
Katibu Mkuu anayesimamia swala za Jinsia na Ushirikiano Anne Wang’ombe, alisema fedha hizo zitagharamia kuwafadhili wanafunzi kutoka kaya zinazopitia changamoto mbali mbali. Alizidi kusisitiza kuwa mpango huo ni mojawapo ya dhamira ya Serikali ya kuboresha maisha ya wasiojiweza na kuongeza ufikaji wa huduma za kifedha.
Wang’ombe alitoa tangazo hilo katika Kaunti ya Kisumu alipoongoza ugawaji wa hundi kwa makundi mbalimbali, mpango ulioandaliwa na Ofisi ya Mwakilishi wa Wanawake, Ruth Odinga.
Takriban wanafunzi 25,000 kote nchini wanatazamiwa kunufaika na mgao huo wa shilingi milioni 273, ambazo zitawasaida katika elimu na ukuzaji wa ujuzi wao.
Kando na hayo, hazina hiyo pia imetoa Shilingi milioni 677 kutekeleza miradi na programu mbalimbali ambazo zitasaidia kukabiliana na ukatili wa kijinsia, kutoa huduma za maji, kukuza vipaji na kutoa huduma zingine zitakazo fanya jamii kustawi.
Kupitia kitita hicho, NGAAF imetenga shilingi milioni 137 kwa ajili ya kuelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu mipango na sera mbalimbali za serikali, ili kuhakikisha wanazipokea programu hizo.