Serikali ya Kenya imetoa hakikisho kuhusu usalama wa usafiri wa angani huku ikitoa salamu za pole kufuatia ajali mbaya ya ndege iliyotokea katika kaunti ya Kwale na kusababisha vifo vya watu wote 11 waliokuwemo.
Kupitia taarifa rasmi, Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir alithibitisha kuwa ndege hiyo, iliyokuwa imesajiliwa nchini Kenya na kuendeshwa na kampuni ya Mombasa Air Safari, ilianguka asubuhi ya Jumanne muda mfupi baada ya kupaa.
Chirchir alisema ndege hiyo yenye nambari ya usajili, 5Y-CCA, iliondoka uwanja wa ndege wa Diani saa 2 na dakika 25 asubuhi ikielekea mbuga ya Maasai Mara.
Hata hivyo, dakika kumi baadaye, saa 2:35 asubuhi, ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na waongozaji wa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa.
Waziri huyo anasema makundi ya dharura kutoka mashirika mbalimbali yalitumwa katika eneo la tukio mara moja na mabaki ya ndege yakapatikana katika wadi ya Tsimba Golini, kaunti ndogo ya Matuga, kaunti ya Kwale.
Watu wote 11 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walithibitishwa kufariki huku ndege hiyo ikiteketea kabisa kufuatia moto uliozuka.
Serikali imeanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Wataalamu kutoka idara ya uchunguzi wa ajali za ndege tayari wamepelekwa eneo la tukio kuanza uchunguzi wa moja kwa moja kwa mujibu wa sehemu ya 13 ya kanuni za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga.
“Serikali ya Kenya inawahakikishia wananchi kuwa usalama wa anga unabaki kuwa kipaumbele chetu cha juu zaidi,” alisema Waziri Chirchir .
“Tumejizatiti kuhakikisha uchunguzi wa wazi, wa kina, na huru, na tutatekeleza hatua zote muhimu kudumisha viwango vya juu zaidi vya usalama wa anga nchini Kenya.”
