Wizara ya Kilimo na ustawi wa mifugo, imetetea hatua yake ya kuwachanja mifugo hapa nchini, ikisema sekta ya mifugo huchangia pakubwa kwa ukuaji wa uchumi wa taifa hili.
Mnamo siku ya Ijumaa akiwahutubia wanahabari, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, alipinga zoezi la kuwachanja mifugo, akisema hatua hiyo itakuwa na athari kubwa za kiafya kwa mifugo hao.
Kupitia kwa taarifa, idara ya ustawi wa mifugo, ilisema kuwa sekta ya mifugo huletea taifa hili asilimia 12 ya pato jumla la taifa, na hivyo ni muhimu kuhakikisha afya bora ya mifugo.
“Mifugo hutekeleza jukumu muhimu katika ukuaji wa uchumi na maisha ya mamilioni ya watu kote duniani. Njia pekee ya kuhakikisha afya bora ya mifugo na usalama katika usambazaji chakula, ni kupitia chanjo ya mifugo,” ilisema idara hiyo.
Baadhi ya manufaa ya kuwachanja mifugo kulingana na idara hiyo ni pamoja na; kuzuia na kudhibiti magonjwa, Kuongeza uzalishaji, uthabiti wa uchumina na kuzuia ueneaji wa magonjwa.
“Madaktari wa mifugo wa serikali na wakulima wanapaswa kushirikiana kuhakikisha mipango ya kuwachanja mifugi inatekelezwa,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha idara hiyo ya ustawi wa mifugo ilisema ni muhimu kutekelezwa kwa zoezi la kuwahamasisha wakulima pamoja na jamii kwa jumla kuhusu umuhimu wa kuwachanja mifugo.
Serikali ilitangaza kuwa itawachanja ng’ombe wote milioni 22 hapa nchini mwezi Januari mwaka 2025. Vilevile ilisema itawachanja mbuzi na kondoo milioni 50 ili kuzuia magonjwa ya mifugo.