Chama cha wafanyabiashara wa bidhaa zinazotokana na zao la Macadamia, kimetoa wito kwa serikali kurejesha marufuku ya uagizaji nje wa zao hilo la Macadamia.
Kulingana na chama hicho, maganda ya Macadamia ni muhimu kwani hutumiwa kama kuni pamoja na kuzalisha kawi kwenye viwanda.
Wakiongea mjini Thika, wanachama wa chama hicho wakiongozwa na Dominic Muraya, walionya kwamba kuuza nje zao hilo la macadamia likiwa na maganda, litanyima viwanda kawi, mbali na kupoteza nafasi za ajira.
Alisema matumizi ya maganda ya macadamia husaidia kuhifadhi misitu kwani hupunguza ukataji miti.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho walisema sehemu ya macadamia hutumiwa kama lishe kwa mifugo, wakidai kuuza nje zao hilo likiwa na maganda pia kutanyima sekta ya kutayarisha lishe ya mifugo malighafi inayohitajika .