Serikali yasimamisha shughuli za wachimba migodi wadogo Migori

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali imeamuru kusimamishwa kwa shughuli zote za wachimba migodi wadogo pamoja na shughuli za wachimba migodi wakubwa wasio na leseni stahiki katika kaunti ya Migori.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki ameyasema hayo baada ya kufanya mkutano na kamati ya usalama ya usalama na ujasusi ya kaunti ya Migori.

Hatua hiyo ilichochewa na ongezeko la visa vya ajali katika migodi ambapo tope huporomoka na kufunika wachimba migodi humo.

Watu wawili walifariki katika hali kama hiyo wiki iliyopita huko Nyatike na wanne wakafariki miezi miwili iliyopita huko Sango.

Kamati ya usalama na ujasusi ya kaunti ya Migori imeelekezwa itekeleze agizo hilo kuhusu wachimba migodi.

Hata hivyo, Waziri Kindiki alisifia juhudi za kamati hiyo katika kutekeleza msako unaoendelea dhidi ya pombe haramu na mihadarati.

Alisema kufikia sasa, misokoto elfu tatu ya bangi imenaswa, washukiwa 106 wamekamatwa na kushtakiwa, sehemu za kuuza pombe 378 zimevamiwa, maduka saba ya kuuza dawa yamefungwa na mengine matano ya dawa za mifugo pia yamefungwa.

Wasimamizi wa masuala ya usalama Migori aidha wamehimizwa kushauriana na wenzao wa kaunti ya Narok ili kutatua mzozo wa umiliki wa ardhi katika eneo la Ntimaru.

Baada ya Migori, Waziri Kindiki alifanya mkutano sawia na kamati ya usalama na ujasusi ya kaunti ya Homa Bay asubuhi ya leo.

Share This Article