Serikali yasema Worldcoin haijasajiliwa nchini Kenya

Martin Mwanje
2 Min Read
Picha kwa hisani ya Nation Media Group

Worldcoin ni kampuni ambayo haijasajiliwa kisheria nchini Kenya. 

Serikali ilisitisha shughuli za kampuni hiyo inayojihusisha na sarafu ya kidijitali mtandaoni humu nchini jana Jumatano huku uchunguzi wa jinai ukianzishwa kubainisha uhalali wa shughuli zake.

Aidha inasema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Worldcoin ni kampuni ambayo imeajiri kampuni mshirika wake humu nchini kwa jina Sense Marketing kuikusanyia data.

“Wawakilishi wa Worldcoin nchini Kenya ni Emmanuel Otieno ambaye ameelezewa kusimamia operesheni za taasisi hiyo na Rael Mwende ambaye ameelezewa kama meneja wa taasisi hiyo nchini Kenya,” walisema Mawaziri Kithure Kindiki wa Wizara ya Usalama wa Taifa na Eliud Owalo wa Habari na Mawasiliano katika taarifa ya pamoja kwa bunge leo Alhamisi.

“Otieno na Mwende wanachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI tangu jana Jumatano, Agosti 2, 2023.”

Mawaziri hao walisema miongoni mwa raia wa kigeni wanaohusiana na kampuni hiyo ni Poitr Piwowarczyk ambaye ameingia nchini mara kadhaa, mara ya mwisho ikiwa Juni 11, 2023 na kuondoka Juni 25.

Walikuwa wakimjibu mbunge wa Manyatta John Mukunji aliyewataka kutoa taarifa kuhusu shughuli ya ukusanyaji data inayofanywa na kampuni hiyo ya kigeni.

Kama hatua ya tahadhari, serikali inasema mamlaka za uhamiaji zimetakiwa kuhakikisha hakuna mtu yeyote ama Mkenya au raia wa kigeni anayehusiana na kampuni hiyo anaondoka nchini bila idhini ya DCI inayoendesha uchunguzi.

Worldcoin ilizua gumzo nchini baada ya maelfu ya raia kujitokeza katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC Jumatatu wiki hii ili kujiandikisha na kampuni hiyo kwa kuchukuliwa data za mboni zao za macho.

Wengi wameelezea mashaka kuhusiana na usalama wa data zilizokusanywa na kampuni hiyo kwa siku tatu hadi jana Jumatano huku wale ambao data zao zilichukuliwa wakilipwa shilingi elfu 7.

Spika wa bunge la Taifa Moses Wetangula sasa amewataka Mawaziri Kindiki na Owalo kufika bungeni Jumatano wiki ijayo ili kuelezea kinagabaubaga wanachokifahamu kuhusiana na shughuli za kampuni hiyo.

Hii ni baada ya wabunge kutoridhishwa na taarifa iliyotolewa na mawaziri hao.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *