Serikali yasambaza pesa za mpango wa Inua Jamii

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali kupitia kwa wizara ya Leba na utunzaji wa jamii imesambaza fedha za mpango wa Inua Jamii za mwezi Disemba mwaka 2023.

Taarifa iliyotiwa saini na waziri Florence Bore inaelezea kwamba fedha hizo ambazo ni bilioni mbili na milioni 9 zilitolewa Ijumaa Disemba 29, 2023.

Milioni 5,930,000 zaidi zilitolewa na wizara hiyo wakati huo kwa ajili ya mpango wa kuboresha lishe kupitia pesa taslimu na mafunzo ya kiafya.

Pesa hizo ziliwekwa kwenye akaunti za benki za watu 1,044,922 ambao wamesajiliwa kwenye mpango wa Inua Jamii ambapo kila mmoja alipokea shilingi elfu 2 za mwezi Disemba mwaka 2023.

Watu hao wanaweza kutoa pesa hizo kwenye akaunti zao kuanzia leo Jumanne Januari 2, 2024.

Mfumo wa kutoa pesa hizo kwa walengwa utabadilika kufuatia agizo la Rais kwamba zitolewe kupitia simu za rununu au ukipenda M-pesa.

Walengwa wa hazina za mayatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na watu wanaoishi na ulemavu wa kiwango cha juu na wahudumu wao watahitajika kujisajili kwa mpango wa M-Pesa.

Awamu ya kwanza ya utoaji wa pesa za hazina hizo mbili tayari imeanza.

Wakongwe ambao wamekuwa wakipokea pesa kutoka kwa wizara hiyo wataendelea kuzipokea kupitia kwa akaunti zao za benki.

Mpango wa serikali wa Inua Jamii unaohusu utoaji wa pesa ulianzishwa kwa lengo la kusaidia walio katika mazingira magumu zaidi katika jamii.

Share This Article