Serikali yasambaza mikopo zaidi kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu

Serikali ilitoa pesa hizo Ijumaa Machi 14, 2025.

Marion Bosire
1 Min Read
Waziri wa elimu Julius Ogamba.

Wizara ya elimu imetangaza kwamba imesambaza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa taasisi za mafunzo ya kiufundi na wale wa vyuo vikuu.

Kulingana na taarifa iliyotolewa leo na waziri wa elimu Julius Ogamba, pesa hizo ambazo ni bilioni 1.56 ni za kugharamia karo na matumizi ya wanafunzi hao.

Pesa hizo zilizotolewa Ijumaa Machi 14, 2025, zilinufaisha wanafunzi 31,263 wa taasisi za mafunzo ya kiufundi na wengine 33,863 wa vyuo vikuu.

Wanafunzi hao wanaripotiwa kupata mawasiliano kuhusu kutolewa kwa fedha hizo kupitia kwa bodi ya utoaji wa mikopo ya kufadhili elimu ya juu HELB.

Mgao huo wa hivi punde unamaanisha kwamba katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025, HELB imesambaza jumla ya shilingi bilioni 32.7 za matumizi na karo kwa wanafunzi 195,522 kwa taasisi za mafunzo ya kiufundi na wengine 390,612 wa vyuo vikuu.

Waziri Migos Ogamba anasema ufadhili huu utahakikisha mahitaji ya wanafunzi na wahadhiri yanatimizwa na hivyo kuwawezesha kuendeleza shughuli za masomo na utafiti bila vikwazo.

Wanafunzi wa vyuo vikuu awali walikuwa wamelalamikia kucheleweshwa kwa ufadhili kutoka kwa serikali wakitishia kufanya maandamano.

Website |  + posts
Share This Article