Serikali yapunguza bajeti kwa shilingi bilioni 132.4

Martin Mwanje
2 Min Read
Serikali imepunguza bajeti ya mwaka huu kwa shilingi bilioni 132.46 kutoka shilingi trilioni 3.981 hadi trilioni 3.848.
Hilo ni punguzo la asilimia 3.3.
Tangazo hilo limetolewa wakati Rais William Ruto alipotia saini kuwa sheria Mswada wa Bajeti ya Ziada 2024 na Mswada wa Ugavi wa Mapato 2024 katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatatu.
Sheria hizo mpya zinawezesha kutolewa kwa rasilimali zitakazochochea ukuaji uchumi na kuboresha utoaji huduma.
Sheria ya Bajeti ya Ziada 2024 sasa inapunguza shilingi bilioni 32.6 kutoka kwa fedha zilizotengewa sekta mbalimbali. Aidha sheria hiyo inaruhusu matumizi ya shilingi bilioni 102 kutoka kwa Mfuko wa Serikali kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, 2024.
Bajeti ya elimu imeongezwa huku elimu ya vyuo vikuu ikipokea shilingi bilioni 4.468 na ile ya sekondari shilingi bilioni 1.112.
Matumizi ya fedha za maendeleo pia yameelekezwa kwa sekta muhimu na kupunguzwa kwa shilingi bilioni 75.29 huku shilingi bilioni 51.12 zikitengewa mahitaji muhimu yanayoibuka.
Fauka ya hayo, shilingi bilioni 3 zimetengewa Idara ya Usalama wa Ndani kwa ajili ya usimamizi wa janga la El Nino na shilingi zingine bilioni 3 kutengewa mpango wa rukuzu wa mbolea.
Na kufuatia mafuriko yaliyoharibu miundombinu, shilingi bilioni 1 zimetengewa ukarabati wa dharura wa barabara.
Kwa upande wake, Sheria ya Ugavi wa Mapato ya 2024 imeongeza fedha zilizotengewa kaunti kwa shilingi bilioni 14.69 kutoka shilingi 385.4 mwaka huu wa fedha hadi shilingi bilioni 400.1 katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mosi.
“Si tu kwamba tumetimiza hitaji la kikatiba la asilimia 15, lakini tumeliongeza kwa asilimia 25,” alisema Rais Ruto wakati wa hafla hiyo.
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *