Wakenya wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali kuondoa rasmi ada ya shilingi 300 iliyohitajika ili kupatiwa vitambulisho vya taifa.
Hatua hiyo imetangazwa na Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen kupitia Gazeti rasmi la serikali lililotolewa leo Jumatano, Machi 19, 2025.
“Ratiba ya Sita ya Sheria za Usajili wa Watu imerekebishwa kwa kuondoa maneno “shilingi 300” yanayoonekana kama ada kwa ajili ya sehemu “Ambao Hawakusajiliwa Awali (NPR) na kubadilishwa na neno “Bila Malipo”, ilisema ilani ya kisheria nambari 59 iliyotolewa na Waziri Murkomen.
Akizungumza wakati wa ziara yake mtaani Kibra wiki jana, Rais William Ruto alitangaza kuwa Wakenya hawatahitajika kulipa malipo yoyote ili kupatiwa vitambulisho vya taifa.
Rais Ruto aliagiza kufutiliwa mbali mara moja kwa malipo ya utoaji vitambulisho hivyo.
“Natangaza nikiwa hapa Kibra ya kwamba, kitambulisho ipatianwe bila malipo yoyote. Kila mtu apatiwe kitambulisho bila malipo na kwa mpango ambao hauna ubaguzi kwa Wakenya,” alisema Ruto.
Agizo hilo la Alhamisi wiki iliyopita lilifutilia mbali agizo la awali, ambapo wanaotafuta stakabadhi hiyo muhimu walihitajika kulipa shilingi 300 na waliopoteza wakitakiwa kulipa shilingi 1,000.
Mwezi uliopita, kiongozi wa taifa akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Kaskazini Mashariki mwa nchi, aliagiza kusitishwa kwa usaili wa wakazi wa mpakani wanaotafuta vitambulisho vya taifa.