Shule zinapoendelea kufunguliwa kwa muhula wa tatu, chama cha walimu wa shule za sekondari na vyuo KUPPET tawi la Meru kinaomba serikali kupitia kwa wizara ya elimu, itoe pesa za kufanikisha uendeshaji wa taasisi za elimu.
Katibu wa chama hicho katika kaunti ya Meru Karuti Nchebere anasema utoaji wa fedha hizo utarahisisha uendeshaji wa shule wanafunzi wanapojiandaa kwa mitihani ya kitaifa.
Akizungumza katika afisi za KUPPET huko Meru, Karuti alisema walimu wakuu wa shule wanakabiliwa na matatizo katika kusimamia taasisi hizo bila pesa kwani wazazi wengi hawana uwezo wa kulipa karo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.
Karuti alisema katika muhula wa kwanza serikali ilitoa asilimia 19 ya pesa hizo, muhula wa pili ikatoa asilimia 18 na hivyo muhula huu wa tatu wanatarajua kwamba itatoa asilimia zaidi ya 60 iliyosalia.
Kiongozi huyo wa walimu alisema muhula wa tatu huwa wa shughuli nyingi walimu wanapotayarisha wanafunzi kwa ajili ya mitihani ya kitaifa kwa hivyo serikali lazima ihakikishe utoaji wa fedha hizo ili kurahisisha mambo.
Alisihi wazazi nao wajibidiishe kulipa karo ya wanao ili kuwezesha usimamizi wa shule kununua vitu kama vyakula ambavyo bei yake imeongezeka maradufu.