Serikali imekanusha kuwepo kwa mkwaruzano wa afisi za kutendea kazi kati Mawaziri Musalia Mudavadi wa Mambo ya Kigeni na mwenzake wa Utumishi wa Umma Moses Kuria.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu wa Mawasiliano kuhusu Mikakati ya Serikali Kibisu Kabatesi amesema habari zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari ni porojo na za kupotosha umma.
Kibisu ameongeza kuwa kulingana na mamlaka, Kuria aliye na mamlaka madogo hawezi kukinzana na Mudavadi aliye na wadhifa mkuu kuhusu afisi.
Taarifa hiyo pia imefafanua kuwa Waziri Mudavadi, amekuwa akifanyia kazi katika jengo la Hazina Kuu kwa muda sasa kusubiri kukamilika kwa ukarabati unaofanyiwa afisi yake katika makao makuu ya Railway lakini tayari amerejea katika afisi yake ya zamani huko Railways huku ukarabati ukiendelea.
Kibisu ameongeza kuwa ugavi wowote wa afisi za kufanyia kazi kwa mawaziri unatekelezwa na Rais na kamwe amri hiyo haiwekezi kubatilishwa na mfanyakazi wa umma.