Serikali yajitolea kufufua mfumo ikolojia

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali imesisitiza kujitolea kwake katika juhudi za ufufuzi wa ikolojia.

Akizungumza kwenye hafla ya wadau, katibu katika wizara ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, Festus Ng’eno alisema uharibifu wa mazingira unaathiri mfumo wa Ikolojia.

Aidha alisema, wakati umewadia kwa kila mmoja kutoa kipaumbele kwa Ikolojia ya maji safi, baharini na nchi kavu.

Ng’eno alisema chini ya malengo ya maendeleo endelevu nambari 15, miito imetolewa kwa mataifa kulinda, kufufua na kuimarisha uendelevu wa matumizi ya Ikolojia ya nchi kavu, usimamizi endelevu wa misitu, kukabiliana na kuenea kwa majangwa pamoja na kusitisha na kuzuia uharibifu wa ardhi sawa na uharibifu wa mimea na wanyama.

Ng’eno alitoa wito kuwepo na matumizi ya mbinu mwafaka za ufufuzi wa Ikolojia.

Msimamizi wa uhifadhi katika shirika la World Wide Fund, Jackson Kiplagat, alisema sekta ya kibinafsi na wanamazingira wanashirikiana na serikali kuu ili kufufua Ikolojia.

Mkutano huo unajiri kabla ya kongamano la 28 la Umoja Wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi litakaloandaliwa mwezi ujao, huko Dubai.

Share This Article