Serikali yahimizwa kuwekeza zaidi katika idara ya utabiri wa hali ya hewa

Marion Bosire
2 Min Read

Mwenyekiti wa kamati ya bunge la taifa kuhusu mazingira, misitu na uchimbaji madini David Gikaria amehimiza serikali kuwekeza zaidi katika idara ya utabiri wa hali ya hewa.

Aliyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mbunge wa kaunti ya Kericho Beatrice Kemei kwenye maadhimisho ya siku ya utabiri wa hali ya hewa ulimwenguni huko Kericho.

Gikaria anahisi kwamba ikiwa na mapato ya kutosha, idara hiyo inaweza kutoa taarifa mapema kuhusu mitindo ya hali ya hewa, taarifa ambazo zitasaidia wakulima kote nchini.

Katika hotuba hiyo, Gikaria alitoa mfano wa mvua ya El-Nino iliyoshuhudiwa nchini mwisho wa mwaka jana na mwanzo wa mwaka huu ambapo anashukuru idara hiyo kwa kuonya wakenya mapema.

Mwenyekiti huyo alihakikishia wizara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu na idara ya utabiri wa hali ya hewa kwamba kamati yake itawaunga mkono.

Mheshimiwa Beatrice Kemei kwa upande wake alishukuru watu wa Kericho kwa kukumbatia ajenda ya serikali kuu ya kupanda miti lengo likiwa miti bilioni 15.

Kiongozi huyo aliomba kwamba vijana wapatiwe kipaumbele katika usambazaji wa miche ya miti kwa ajili ya upanzi kutoka kwa serikali kuu.

Alisema wengi wa vijana hao hawana ajira na wakipatiwa fursa hiyo watajipatia riziki.

Siku ya utabiri wa hali ya hewa ulimwenguni huadhimishwa tarehe 23 mwezi Machi kila mwaka tangu mwaka 1951.

Share This Article