Serikali ya kitaifa kupitia kwa wizara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu, imesisitiza kuhusu umuhimu wa kuendeleza shughuli za kuhifadhi misitu chini ya mipango ya PELIS hasa baada ya visa vya moto kwenye misitu.
Akihutubia wanachama wa muungano wa uhifadhi wa misitu huko Kinangop, afisa anayesimamia misitu katika kaunti ya Nyandarua Bernard Nguya, aliangazia athari mbaya za visa vya moto katika eneo hilo.
Zaidi ya ekari elfu tano za eneo la msitu ziliharibiwa na moto na hivyo kusababisha haja ya juhudi za haraka za kurejesha eneo hilo.
Nguya alipongeza mpango huo huku akiomba makundi husika kusalia imara na kuendeleza mipango ya kuafikia lengo la kuongeza eneo la misitu nchini, alivyoagiza Rais William Ruto.
Misitu ni muhimi katika kusawazisha mfumo ikolojia kwa kutoa makazi kwa wanyamapori, kudhibiti mzunguko wa maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Nchini Kenya, serikali imeweka lengo la kuongeza eneo la misitu hadi asilimia 10 kufikia mwaka 2030, kutoka eneo la sasa ambalo ni asilimia 7.
Ili kuafikia lengo hili juhudi za kudumu zinahitajika, ikiwa ni pamoja na upanzi wa miti, uendelezaji wa misitu, na usimamizi madhubuti wa misitu iliyopo.
Mipango yaPELIS ni sehemu muhimu ya mkakati huu, ambapo inawezesha jamii za mitaa kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na usimamizi wa misitu.
Mbali na manufaa yao kwa mazingira, misitu inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo jamii zinategemea misitu kwa rasilimali kama vile kuni, mimea ya dawa, na mbao.
Kwa kuhakikisha kuwa eneo la misitu linadumishwa na kuboreshwa, serikali inalenga kuongeza uendelevu wa kimazingira na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Msaada wa vikundi vya mitaa na ushiriki endelevu wa wadau utakuwa muhimu katika kufikia malengo haya na kuhakikisha mustakabali bora na endelevu kwa misitu ya Kenya.