Serikali imefunga takriban vituo 6,000 vya kuuzia pombe nchini huku msako dhidi ya pombe haramu ukiendelea kushika kasi.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Wizara ya Usalama wa Taifa ilisema vituo hivyo vimefungwa baada ya kubainika kwamba havikufuata kanuni zilizowekwa kisheria.
Vituo hivyo ni kati ya karibu vituo 48,000 vilivyokaguliwa wakati wa msako huo.
Wizara imesema eneo la Bonde la Ufa limerekodi idadi kubwa ya vituo vilivyoruhusiwa kuendelea kuhudumu.
Aidha eneo la Mashariki lilifuatia kisha maeneo ya Kati, Nyanza, Magharibi, Pwani na hatimaye eneo la Kaskazini Mashariki.
Kwa mujibu wa Wizara, asilimia 86 ya vituo vilivyokaguliwa vimekidhi viwango vilivyowekwa.
Msako huo wa kitaifa unaoongozwa na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki, unanuia kuwakabili wauzaji pombe haramu na wanaochangia matumizi ya dawa za kulevya nchini.