Serikali yafunga kambi ya waathiriwa wa mafuriko Maai Mahiu

Tom Mathinji
1 Min Read

Serikali imeanza mchakato wa kufunga kambi za waathiriwa wa mafuriko yaliyotokea Maai Mahiu, zilizobuniwa kuhifadhi familia zilizopoteza makao.

Hatua hii inalenga kuwezesha familia hizo, kuanza upya maisha yao wiki tatu baada ya mkasa huo.

Mwishoni mwa wiki jana, kamati ya usimamizi wa mkasa huo, iliandamana na waathiriwa wa mkasa huo waliokuwa wakiishi katika makao ya watoto ya PBB, kutambua wamiliki halali wa ardhi, iliyoathiriwa na mafuriko.

Miongoni mwao ni familia 11 ambazo nyumba zao hazikusombwa lakini zilizama, ambazo zimeagizwa kurejea katika nyumba zao mara moja.

Kwa upande mwingine, wamiliki wa nyumba ambazo zilisombwa na maji, wanadai kuwa walipewa makataa ya wiki mbili kutafuta na kuhamia nyumba za kukodisha katika eneo hilo.

Kila familia ilitarajiwa kuokea shilingi 5,000 kulipia kodi kwa muda wa miezi mitatu, fedha ambazo familia hizo zinasema hazitoshi.

Familia 46 zilikuwa zimehifadhiwa katika kambi ya PBB camp, huku familia nane zikitarajiwa kurejea katika nyumba zao mwishoni mwa wiki hii.

Share This Article