Serikali yaanzisha mafunzo kwa makamishna wa maeneo na kaunti

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu katika Wizara ya Mambo ya Ndani Dkt. Raymond Omollo leo Jumatatu ameanzisha rasmi mpango wa mafunzo kwa makamishna wa maeneo na wale wa kaunti katika taasisi ya mafunzo ya serikali, KSG katika eneo la Lower Kabete.

Akizungumza katika hafla hiyo, Omollo alisema serikali inalenga kuhakikisha mabadiliko mwafaka katika utendakazi wa wawakilishi wa serikali kuu mashinani na hivyo ni muhimu maafisa hao wapokee ujuzi wanaohitaji ili kuboresha kazi zao.

Aliongeza kuwa maafisa wa serikali kuu mashinani lazima wahakikishe kwamba mtagusano wao na wananchi unafanyika kwa wakati unaofaa, wawe na taarifa sahihi na wawe na uelewa wa mahitaji ya wananchi wanaosimamia.

Kulingana naye, mpango huo wa mafunzo unawiana na marekebisho yaliyofanyika hivi maajuzi serikalini na mabadiliko katika namna ya usimamizi.

“Serikali inapoongeza kasi hatua kwa hatua katika utekelezaji wa nguzo yake ya maono ya kuboresha uwezo wa kiuchumi wa wananchi kupitia mpango wa Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu – BETA, ni lazima maafisa wanaoiwakilisha mashinani waelewe mpango huo na athari zake,” alisema Omollo.

Alisisitiza kujitolea kwa serikali kuimarisha utendakazi na usimamizi wa utekelezaji wa mipango yake ili iweze kutatua ipasavyo mambo kama amani, usalama na mabadiliko ya tabia nchi.

Omollo alitoa changamoto kwa maafisa wa serikali kuu mashinani waongoze katika kuendesha mikutano ya kuhusisha wananchi kabla ya utekelezaji wa miradi ya serikali ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji.

Aliwaonya vikali maafisa hao dhidi ya ufisadi akisema hauruhusiwi kamwe katika utedakazi wa serikali.

Share This Article