Serikali yaahidi kushughulikia matakwa ya walimu

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali imeahidi kushughulikia malalamishi yote ya walimu huku ikipongeza chama cha walimu KNUT kwa kufutilia mbali mgomo ambao ungeanza leo Agosti 26, 2024.

Waziri wa Elimu Julius Migosi Ogamba katika taarifa aliwashukuru maafisa wakuu wa chama cha KNUT kwa kufutilia mbali mgomo na kusisitiza kujitolea kwa serikali kushughulikia walimu.

Wakati huo huo waziri huyo amewataka wazazi na walezi wa watoto kuhakikisha kwamba wamerejea shuleni ilivyokuwa imepangwa awali.

Alisema wizara tayari imetoa shilingi bilioni 21.8 za kugharamia elimu katika taasisi za elimu ya msingi ili kufanikisha kurejelewa kwa masomo humo kwa muhula wa tatu.

“Tutatumia mfumo wa majadiliano na wadau wote na kushirikiana ili kuafikia jibu mwafaka kwa masuala yote yanayowasibu walimu.” alisema waziri Migosi akiongeza kwamba hatua hiyo itaboresha mazingira ya kikazi kwa walimu.

Baada ya mkutano wa viongozi wake wakuu, KNUT ilitangaza jana Jumapili kwamba imetupilia mbali mgomo kwani masuala yaliyosalia yatatatuliwa kwa njia ya kiusimamizi.

Kutokana na hilo, walimu ambao ni wanachama wa KNUT walielekezwa warejee kazini leo Jumatatu Agosti 26, 2024 wakati ambapo shule zinaanza kufunguliwa kwa muhula wa tatu.

Kujitolea kwa serikali kushughulikia matakwa ya walimu yanayojumuisha kuajiriwa kwa walimu zaidi na wanaohudumu kama wanagenzi waajiriwe kwa masharti ya kudumu ndiko kulichochea KNUT kufutilia mbali mgomo.

Hata hivyo chama cha walimu wa shule za upili na vyuo KUPPET kinasisitiza kwamba mgomo unaanza leo kama walivyotangaza awali.

Share This Article