Serikali ya kaunti ya Kilifi imeelezea masikitiko yake kutokana na kifo cha Rahab Amani Karisa ambaye hadi kifo chake, alikuwa Afisa Mkuu aliyesimamia kitengo cha Uchumi wa Baharini katika Idara ya Kilimo, Ustawi wa Mifugo na Uchumi wa Baharini.
Gavana Gideon Mung’aro katika taarifa amemuelezea marehemu kama mtu aliyekuwa kijana, mwenye kipaji, mchapa kazi, na ambaye mustakabali wake ulikuwa mzuri.
“Kulingana na uchunguzi wa awali wa polisi, Rahab aliuawa na yaya wake. Natoa wito kwa taasisi za upelelezi kuchukua hatua za haraka na kumkamata mshukiwa ili akabiliane na sheria kikamilifu,” alisema Gavana Mung’aro katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi mchana.
Aliongeza kuwa serikali yake itafanya kazi kwa karibu na familia kupanga mazishi ya mwenda zake.
Karisa anasemekana kuuawa kwa kudungwa kisu na mhudumu wake wa nyumbani katika eneo la Mnarani, kaunti ya Kilifi leo Alhamisi asubuhi.
Alirejea kutoka nchini Italia jana Jumatano ambako alikuwa amekwenda kwenye ziara.
Yaya huyo aliripotiwa kutoroka kabla ya kuwasili kwa walinzi wa kibinafsi baada ya kutekeleza kitendo hicho cha kinyama.
Maafisa wa polisi kwa sasa wanachunguza kisa hicho.