Serikali ya kaunti ya Embu inapanga kwenda mahakamani kupinga hatua ya serikali za kaunti za Mombasa na Kilifi ya kupiga marufuku uuzaji na matumizi ya Muguka.
Naibu Gavana wa kaunti ya Embu Kinyua Mugo anasema serikali hiyo tayari imepata mawakili ambao wanatizamiwa kuweka kesi mahakamani kesho Jumatatu.
Mugo alisema kupitia taarifa kwamba hatua yao ya kwanza ni kutafuta maagizo ya mahakama ya kuondoa marufuku hiyo huku wakitafuta namna ya kusuluhisha zogo lililopo kuhusu Muguka.
Anasema hakuna sababu yoyote ya kupiga marufuku Muguka katika kaunti hizo mbili huku miraa ikikubaliwa humo.
Naibu huyo wa Gavana anahisi kwamba wahusika wote wa ukuzaji, usambazaji na matumizi ya Muguka wataathiriwa vibaya na marufuku hiyo huku kaunti husika zikipoteza pesa ambazo kwa kawaida hukusanywa kama ushuru kutoka kwa biashara ya Muguka.
Kulingana na Mugo huenda kuna njama fiche kwani marufuku ya Muguka inajiri siku chache tu baada ya Gavana wa Embu Cecily Mbarire kukutana na mwenzake wa Mombasa Abdulswamad Shariff kuzungumzia uthibiti wa biashara ya Muguka na Miraa.
Alisema hakuna ushahidi wa kisayansi wa kudhihirisha kwamba Muguka ni dawa ya kulevya na hakuna sheria inayozuia uuzaji na matumizi yake nchini Kenya.