Serikali ya kaunti ya Kakamega, imesema itaimarisha ushirikiano wake na shirika la kimataifa la misaada la Marekani USAID, kutekeleza miradi ya maendeleo katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa warsha ya siku ya washirika wa USAID iliyoandaliwa katika hoteli moja kwenye kainti hiyo, Barasa alipongeza shirika hilo kutokana na miradi ambayo imetekeleza kwenye kaunti hiyo.
Alisema anatazamia ushirikiano zaidi kutoka washirika zaidi wa maendeleo, kuimarisha miundombinu kamavile mabomba ya kupitisha majitaka na usafi, huku kaunti hiyo ikijizatiti kuwa Jiji la sita hapa nchini.
“Hivi karibuni tutazindua manispaa tatu, Malava, Butere na Matunda. Maeneo ambayo tunalenga kuwa na ushirikiano na uimarishaji wa miundo mbinu kama vile mabomba ya kupitisha maji taka, hatuwezi kuwa Jiji iwapo hakuna mfumo bora wa mabomba hayo,” alisema Barasa.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa USAID nchini Kenya na Afrika Mashariki Bert Ubamadu, alidokeza kuwa serikali ya Marekani imekuwa na ushirikiano na Kenya kwa zaidi ya miaka 60, kupiga jeki miradi ya maendeleo hapa nchini.
Mkurugenzi huyo alisema USAID inashirikiana kwa karibu na Gavana wa Kakamega na kundi lake kuboresha sekta ya afy, mipango ya elimu kwa wanafunzi wa gredi ya 1 hadi 3, Maji na usafi na katika sekta ya kilimo.