Serikali ya kaunti ya Homa Bay ilikusanya mapato yenye kima cha shilingi milioni 101.6 mwezi Septemba, 2023.
Seikali hiyo inayoongozwa na Gavana Gladys Wanga ilikusanya jumla ya shilingi milioni 291.5 katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023-2024.
Haya yalibainika katika ripoti iliyozinduliwa wakati mkutano wa kuangazia mapato yaliyokusanywa mwezi Septemba na kuhudhuriwa na Gavana Wanga.
Kuendana na mpango wa kufikia asilimia 100 ya ukusanyaji ushuru kwa njia ya dijitali, kaunti ya Homa Bay imeanzisha mpango wa ukaguzi wa ghala za pombe na vituo vya uuziaji pombe hiyo ili kuboresha mchakato wa utoaji leseni.
Lengo ni kuongeza ukusanyaji ushuru na hivyo kupanua wigo wa mapato yanayokusanywa kwa kusudi la kufanikisha utekelezaji miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi.