Serikali inalenga kuondoa pikipiki 13,000 zinazotumia mafuta ya petroli ambazo hutumiwa na machifu na manaibu wao, huku zikibadilishwa na zile zinazotumia nguvu za umeme.
Hayo ni kulingana na katibu katika wizara ya usalama Dkt. Raymond Omollo.
Omollo alisema hatua hiyo ni mojawepo wa juhudi za serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi mashinani.
Omollo aliyasema hayo Jumatatu afisini mwake katika jumla la Harambee, alipozindua awamu ya kwanza ya pikipiki 22 zinazotumia umeme.
Aidha alidokeza kuwa pikipiki hizo zinazotumia umeme, zitaimarisha usafiri wa Machifu hao na Manaibu wao, wanapotekeleza majukumu yao.
“Chini ya mpango huu mpya, tumeanzisha mradi wa majaribio wa pikipiki zinazotumia umeme katika kaunti za Machakos, Kiambu, Nairobi na Kajiado, kwa kusambaza pikipiki 22 kwa Machifu,” alisema Omollo.
Omollo alisema pikipiki zaidi za umeme zitasambazwa kwenye awamu ya majaribio itakayoendelea kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kuanza usambazaji pikipiki hizo kwa awamu kwa machifu wote na manaibu wao nchini.
Alitoa wito kwa sekta ya kibinafsi hasaa ile ya pikipiki, kukumbatia pikipiki hizo zinazotumia nguvu za umeme.