Serikali itawaajiri wahamasishaji wa afya ya jamii 103,000 katika hatua ambayo itasaidia kuokoa maisha na rasilimali.
Rais William Ruto amesema wahamasishaji hao watapewa vifaa tiba vya kisasa na kutumwa kuhudumu katika jamii kote nchini.
Ruto aliyasema hayo alipokutana na Msimamizi wa shirika la USAID katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano.
USAID itasaidia katika kutoa mafunzo kwa wahamasishaji hao.
Rais Ruto ameipongeza M-Mama, programu bunifu ya kutoa huduma za ambulensi kwa kutumia simu ya mkononi ambayo kina mama wajawazito na kina mama waliojifungua kwa mara ya kwanza wanaweza wakapiga kutafuta usaidizi wanapokuwa taabani.