Serikali kuu yatenga shilingi bilioni 7 kupambana na athari za mafuriko

Martin Mwanje
1 Min Read

Jumla ya shilingi bilioni 7 zimetengwa na Baraza la Mawaziri kukabiliana na athari za mafuriko katika maaeneo yaliyoathiriwa zaidi. 

Shilingi bilioni 2.4 kati ya shilingi hizo zilitolewa wiki jana ili kununua chakula na bidhaa zingine kwa ajili ya matumizi ya waathiriwa wa mafuriko hayo katika maeneo kame.

Kaunti za kaskazini mashariki mwa nchi zimeathirika mno na mafuriko huku maelfu ya wakazi wakiachwa bila makazi.

Viongozi wa kaunti hizo wamekuwa wakipaza sauti wakiitaka serikali kuu kuingilia kati haraka kabla ya mambo kwenda mrama.

Msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed alidokeza hayo alipowahutubia wanahabari kuhusiana na mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi kuangazia hali ya mafuriko nchini.

Alitoa wito kwa serikali za kaunti kupiga jeki jitihada zinazofanywa na serikali kuu za kukabiliana na athari za mafuriko kwa kutenga fedha za kukabiliana na hali hiyo kutoka kwenye bajeti zao.

Serikali za kaunti siku zilizopita zimeilaumu serikali kuu kwa kukosa kutoa fedha za dharura za kukabiliana na athari za mafuriko yanayoshuhudiwa nchini.

 

 

Share This Article