Serikali kutekekeza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William Ruto leo Alhamisi, ameongoza mkutano wa baraza la mawaziri kwa mara ya pili wiki hii ili kujadili hatua za ziada za kusaidia kukabiliana na athari za mafuriko na maporomoko ya ardhi hapa nchini.

Katika taarifa, baraza la mawaziri liliarifiwa kuwa wakenya zaidi wanafikiwa na kusaidiwa na vyakula na bidhaa nyingine za kimsingi.

Baraza la Mawaziri lilibaini kuwa athari mbaya za mafuriko na maporomoko ya ardhi na udongo katika maeneo mengi nchini, yameathiri vibaya maisha ya wakenya wengi.

Huku likitambua kuwa mafuriko, maporomoko ya udongo na ardhi na hali nyingine mbaya za hali ya hewa yanasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, baraza la mawaziri liliazimia kuwa serikali kuanzia sasa itaongoza taifa katika kutekeleza mipango maalum na sera za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Baraza la Mawaziri lilifahamishwa kuhusu utabiri wa hali ya hewa kwa miezi mitatu ijayo, unaoonyesha kuwa mvua zitaendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi.

Baraza la Mawaziri liliarifiwa kwamba athari za Kimbunga Hidaya mara tu kinapotua katika Pwani ya Tanzania zinaweza kusambaa hadi katika eneo la pwani ya Kenya.

Wizara ya Elimu iliagizwa kuweka mikakati ya ukarabati wa miundo misingi ya shule ambazo ziliathiriwa na mafuriko.

TAGGED:
Share This Article