Serikali kushirikiana na vyuo vikuu kuimarisha usalama wa chakula

Tom Mathinji
2 Min Read

Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, amesema serikali itashirikiana na vyuo vikuu, wabunifu na sekta ya kibinafsi kuimarisha uwezo wa taifa hili kujitosheleza kwa chakula kupitia utafiti na teknolojia.

Akizungumza wakati wa maonyesho ya kilimo ya kaunti ya Uasin Gishu yaliyoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Eldoret, Dkt. Rono alikariri kujitolea kwa serikali kuwapiga jeki wakulima katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kukumbatia teknolojia, kuboresha usimamizi wa baada ya mavuno na kuimarisha uongezaji thamani.

“Wizara ya Kilimo itashirikiana na vyuo vikuu, wabunifu na sekta ya kibinafsi kuboresha utumizi wa teknolojia kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, uzalishaji chakula kupitia mbinu za kisasa, utunzaji wa udongo na utumizi wa mbegu bora,” alisema Dkt. Ronoh.

Dkt. Ronoh alisema Wizara ya Kilimo itatekeleza hayo kupitia mpango mpya wa Mama Kitchen Garden, unaolenga kuwafaidi wanavijiji 24,000 kote nchini.

Kupitia mpango wa Mama Kitchen Garden, wakulima wadogo wadogo watafaidika na miradi ya usambazaji maji, pembejeo za kilimo, mafunzo na hamasisho, ili kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na utumizi bora wa ardhi.

Kulingana na katibu huyo, mpango huo mpya utasaidia taifa hili kutumia vyema ardhi iliyopo, ambayo inaathiriwa kila uchao na ongezeko la idadi ya watu.

Aidha amesema serikali itaanza kusambaza mbolea ya bei nafuu kwa wakulima kuanzia mwezi Novemba kupitia Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), maduka ya kuuza dawa za kilimo, mashirika ya wakulima na vyama vya akiba na mikopo.

Serikali pia itahakikisha wakulima wanapata mbegu bora na dawa za kuwaangamiza wadudu zilizoidhinishwa.

Share This Article