Serikali inajizatiti kununua na kusambaza magunia Milioni 12.5 ya mbolea za bei nafuu kwa wakulima Milioni 6.5 kote nchini, wakati huu wa msimu wa upanzi.
Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, amesema serikali tayari imenunua magunia Milioni tano ya mbolea, zitakazotumika wakati huu wa msimu wa mvua.
Ronoh aliyasema hayo Jumatano alipozindua mpango wa pili wa kimkakati wa shirika la utafiti wa kilimo na mifugo KALRO), utakaodumu kwa muda wa miaka mitano.
“Wiki iliyopita tulizindua magunia Milioni moja ya mbolea kutoka kwa bandari ya Mombasa, ambayo kwa sasa imesambazwa katika maghala ya halmashauri ya nafaka na mazao NCPB kote nchini,” alisema katibu huyo.
Hata hivyo alisikitika kuwa wakulima hawapati mbolea ya ubora unaohitajika, kulingana na utafiti uliofanywa na KALRO.
Katibu huyo alisema walioshiriki katika kusambaza mbolea bandia kwa wakulima, tayari wamekamatwa na leseni za viwanda vyao kufutiliwa mbali, wakisubiri mfumo wa sheria kuchukua mkondo.
“Tutahakikisha washukiwa hao wamechukuliwa hatua, ili wakulima wapate haki. Baadhi yao walijaribu kutoroka, lakini serikali ilikuwa macho katika mipaka yote,” alidokeza Ronoh.