Katika hatua inayokusudiwa kusaidia wakenya wanaokabiliwa na dharura za afya ughaibuni, serikali imesisitiza kujitolea kusaidia waliokwama ughaibuni kwa kukosa ada ya hospitali.
Haya yanajiri wakati ambapo wakenya milioni 14 wamejisajili kwenye mamlaka inayosimamia afya ya jamii SHA.
Waziri wa Afya Deborah Barasa aliyasema hayo katika mkutano na wanahabari baada ya mahafali ya wauguzi spesheli 39 katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya chuo kikuu cha Kenyatta – KUTRRH.
Aliahidi kwamba kila kisa cha mgonjwa aliyekwama ughaibuni kwa sababu ya bili za hospitali kitashughulikiwa kando, hatua inayowapa matumaini wengi wanaokabiliwa na tatizo hilo.
Akizungumzia wasiwasi ulioibuliwa kuhusu mpito kutoka NHIF hadi SHIF Barasa alisisitiza kwamba mgogoro unaodhaniwa kuwepo umefanywa kuonekana kuwa mkubwa zaidi ya ulivyo.
Aliomba wakenya kufahamu ukweli na uongo akiongeza kusema kwamba ripoti zinazotolewa hazionyeshi hali halisi za mfumo huo mpya.
Wauguzi waliohitimu leo mbele ya mkurugenzi mkuu wa hospitali ya KUTRRH Ahmed Dagane na mwenyekiti wa bodi Olive Mugenda, walitunukiwa vyeti vya diploma ya juu katika nyanja mbali mbali za uuguzi.
Akiangazia mafanikio ya SHIF waziri Barasa alizungumzia hali katika hospitali hiyo ya chuo kikuu cha Kenyatta ambapo mfumo wa bima hiyo mpya ya afya ya jamii umegharamia shilingi milioni moja kwa kila mgonjwa.
Daktari Barasa aliomba ushirikiano uwepo kati ya vyuo vikuu, hospitali na taasisi nyingine za kozi za utabibu ili kuimarisha uvumbuzi na kuinua viwango vya afya.