Serikali inalenga kuongeza ukuzaji wa mimea inayozalisha mafuta ya kupika kutoka ekari 150,000 hadi ekari milioni nne kufikia mwaka 2027.
Hatua hii inalenga kupunguza uagizaji wa mafuta hayo ya kupikia kutoka mataifa ya nje.
Akizungumza leo Jumanne katika maonyesho ya kilimo yanayoendelea katika kaunti ya Bungoma, katibu katika wizara ya kilimo Jonathan Mueke, alisema shilingi milioni 981 zimetolewa na hazina kuu kwa ushirikiano na halmashauri ya kilimo na chakula AFA kufadhili mradi ulioanzishwa na serikali wa kupigia debe ukuzaji wa mimea inayozalisha mafuta ya kupikia.
“Mradi huu ulianza Julai 1,2023 katika maeneo ya Rift Valley, Magharibi, Mashariki na Pwani kuchochea ukuzaji wa alizeti, Maharagwe aina ya Soya na Nazi,” alisema katibu Mueke.
Kulingana na Mueke, hatua hiyo ni mojawapo ya mikakati inayotekelezwa na serikali, kuhakikisha taifa hili lina chakula cha kutosha.
Aidha alisema uzalishaji wa mafuta ya kupikia, utapunguzia taifa hili gharama kubwa ya uagizaji bidhaa kutoka nje, ambayo kwa sasa ni shilingi bilioni 100 kwa mwaka.
Maonyesho hayo ya kilimo ambayo yameandaliwa na wizara ya kilimo na ustawi wa mifugo katika chuo kikuu cha Kibabii, yamewaleta pamoja wadau mbali mbali katika sekta ya kilimo, kwa lengo la kuhamasisha kuhusu kufanikisha usalama wa chakula hapa nchini.