Waziri wa Usalama wa taifa Profesa Kithure Kindiki, anasema serikali inapanga kuweka amri ya kupiga marufuku watu kutoka nje wakati usiku katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini Mashariki ili kudhibiti ongezeko la visa vya ujambazi.
Profesa Kindiki anasema vyombo vya usalama vitaendesha operesheni ya usalama katika eneo la mashariki, operesheni sawa na inayoendelea katika eneo la kaskazini mwa Rift Valley ili kudhibiti visa vya ujambazi.
Akizungumza huko Ndumuru, eneo bunge la Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru, Waziri huyo alisema atatangaza maeneo hayo ili kuweka amri ya kutotoka nje na shughuli zingine za usalama.
” Kuanzia juma lijalo, serikali itaanzisha operesheni za kiusalama katika baadhi ya maeneo ya Mashariki mwa nchi, kama sehemu ya operesheni inayoendelea ya maliza uhalifu katika eneo la Rift Valley,” alisema waziri Kindiki.
Prof. Kindiki, ambaye aliongoza hafla ya kufuzu kwa Askari wa Kitaifa wa Akiba wapatao 140 katika Kaunti ya Meru, aliwaagiza maafisa hao wapya kusalia katika kambi hiyo na kulinda wakazi na mifugo, akisema kuwa polisi watapelekwa katika mpaka wa Kaunti za Isiolo na Meru ili kuimarisha usalama.
Seneta huyo wa zamani wa Tharaka Nithi alidokeza kuwa wizi wa mifugo umekithiri katika eneo hilo, akisema kuwa serikali imechukua hatua sawia na zile ilizochukua katika maeneo mengine kutokomeza jinamizi hilo.