Vikosi vya usalama katika eneo la North Rift, vimeimarisha juhudi za kumaliza wizi wa mifugo na aina zingine za uhalifu ambazo zimeghubika eneo hilo kwa miongo kadhaa.
Waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki alisema, licha ufanisi mkubwa kushuhudiwa Katika kukabiliana na majangili hao, serikali haitalegeza kamba hadi wezi wa mifugo waangamizwe kabisa.
Ili kufanikisha hayo, waziri huyo alidokeza kuwa serikali inapanga upya usimamizi wa kikosi cha polisi wa akiba hapa nchini NPR, ili kupiga jeki juhudi za huduma ya taifa ya polisi-NPS na kikosi cha ulinzi cha Kenya KDF.
Aliyasema hayo baada ya kushiriki mkutano wa kiusalama na makamanda na viongozi wa usalama wa eneo hilo katika shule ya msingi ya Ngaratuko, Baringo kaskazini, kaunti ya Baringo siku ya Jumanne, wakati wa kutathmini na kukagua msako wa kiusalama unaoendelea, ili kuepusha visa vya ujambazi na wizi wa mifugo.
Alikariri kwamba kuanzishwa kwa kituo cha polisi wa akiba katika eneo hilo ni muhimu katika kukabili vitisho vinavyotokana na majambazi katika eneo la kaskazini ya Rift Valley.