Serikali kuimarisha maendeleo kwenye maeneo ya wafugaji

Murkomen alidokeza kuwa visa vya ujangili na wizi wa mifugo, vimechochewa pakubwa na kutengwa kimaendeleo kwa maeneo ya wafugaji.

Tom Mathinji
1 Min Read
Kipchumba Murkomen - Waziri wa Usalama wa Taifa.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema serikali itatekeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo ya wafugaji, kwa lengo la kukabiliana na zimwi la ujangili na wizi wa mifugo.

Akizungumza alipokutana na viongozi kutoka kaunti ya Isiolo, Murkomen alidokeza kuwa visa vya ujangili na wizi wa mifugo, vimechochewa pakubwa na kutengwa kimaendeleo kwa maeneo ya wafugaji.

“Wanaotekeleza maovu hayo ni waathiriwa wa ukosefu wa maendeleo. Suluhu la kudumu kwa changamaoto hilo ni kuongeza ujenzi wa barabara katika maeneo hayo,” alisema Murkomen.

Waziri huyo alisema ili kuimarisha hali ya usalama katika kaunti hiyo, serikali inatoa mafunzo na kuwapeleka maafisa zaidi wa polisi wa akiba (NPRs), kufungua vituo zaidi vya polisi, kubuni kambi za polisi na kupeleka vifaa zaidi vya usalama katika maeneo ambayo yanakabiliwa na wizi wa mifugo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na naibu gavana wa Isiolo  James Lowasa, mbunge wa Isiolo Kaskazini  Joseph Samal, na wawakilishi wadi miongoni mwa viongozi wengine.

Share This Article