Idadi ya waliofariki kutokana na Ebola yafika 4,000 DRC

Wataalam wamesema miundombinu hafifu ya afya na ghasia zinazoendelea, zimehujumu juhudi za kukabiliana kikamilifu na ugonjwa huo.

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu 4,000 wafariki kutokana na Ebola DRC.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imenakili zaidi ya visa 8,000 vya ugonjwa wa Ebola, huku takriban watu 4,000 wakifariki kutokana na makali ya ugonjwa huo, katika kile kimetajwa kuwa maambukizi mabaya zaidi ya Ebola kwenye historia ya nchi hiyo.

Kulingana na takwimu zilizochapishwa na Wizara ya Afya ya DRC siku ya Jumatatu, watu 8,067 ⁠⁠wameambukizwa ugonjwa huo na wagonjwa ⁠⁠3,901 wamefariki, hii ikiwakilisha asilimia 48.4 ya vifo kutokana na Ebola.

Hadi kufikia sasa chanjo kadhaa zinatumika katika matibabu ya virusi hivyo aina ya Bundibugyo, ambapo bado hakuna chanjo au matibabu yaliyoidhinishwa kukabiliana na maambukizi yake.

Wataalam wamedokeza kuwa miundombinu hafifu ya afya na ghasia zinazoendelea kwenye mipaka ya DRC na Sudan Kusini, Uganda na Rwanda, zimehujumu juhudi za kukabiliana kikamilifu na ugonjwa huo.

Juma lililopita, Marekani ilitangaza kutoa msaada wa dola milioni 267 zaidi, kupiga jeki vita dhidi ya Ebola.

Share This Article