Serikali itaifanya Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS kuwa ya kisasa kwa gharama ya shilingi bilioni 28 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Hayo yamesemwa na Rais William Ruto ambaye ameongeza kuwa mpango huo utajumuisha ununuzi wa vifaa na silaha mpya, kuzifanya shughuli za polisi kutolewa kwa njia ya dijitali na pia ujenzi wa nyumba mpya za maafisa wa polisi.
“Nataka kuahidi kuwa nakusudia kusimamia mchakato wa kuifanya huduma hiyo kuwa ya kisasa hadi umalizike katika kipindi cha miaka miwili ijayo ili tuweze kuwa na vifaa, magari na silaha zinazohitajika kuilinda nchi yetu,” amesema kiongozi wa nchi.
Aliyasema hayo alipozindua mipango ya kimkakati ya NPS na Idara ya Urekebishaji Tabia ya mwaka 2023-2027 katika Shule ya Mafunzo ya Serikali, KSG katika eneo la Lower Kabete, Nairobi.
Hadi kufikia sasa, Rais amesema serikali imetumia shilingi bilioni 2 kuongeza viwango ndani ya huduma hiyo.
Ameongeza kuwa polisi watanunuliwa magari mapya 1,000 mapema mwaka ujao chini ya mpango wa polisi wa kukodi magari katika juhudi za kukabiliana na uhaba wa magari katika vituo vya polisi kote nchini.
Rais amesema mipango inaendelea ya kununua magari 2,000 zaidi.
Na ili kuimarisha hali ya maisha ya maafisa wa polisi, Rais Ruto amesema nyumba mpya 582 zimejengwa wakati zingine 1,000 zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Serikali inakusudia kujwaengea maafisa wa polisi nyumba mpya 17,000.