Serikali itaunga mkono ufufuzi wa kampuni ya sukari ya Nzoia.
Rais William Ruto amesema serikali itaifadhili kampuni hiyo kupata vifaa vya kisasa vya utendakazi na kuachana na matumizi ya vile vilivyozeeka.
Rais amesema serikali aidha itatoa fedha za kupiga jeki upanzi wa miwa katika eneo la kampuni hiyo linalojulikana kama Nucleus Estate.
Alisema hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa miwa wa kampuni hiyo na uwezo wa kusaga miwa ili kuboresha utendakazi wake kikamilifu.
“Tunataka kuhakikisha utendakazi wa kampuni hii unaimarika, tunachochea ukuaji uchumi na kuongeza nafasi za ajira kwa watu wa Nzoia na viunga vyake,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa serikali itabadili usimamizi wa kampuni hiyo kwa kuweka usimamizi wa kitaalam na wa kibinafsi.
“Tunaenda kuwa na usimamizi mpya ambao utatoa kipaumbele kwa maslahi ya umma na wakulima,” alisema kiongozi wa nchi.
Alizungumza hayo alipoitembelea kampuni ya sukari ya Nzoia katika kaunti ya Bungoma akiwa ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na Gavana wa Bungoma Ken Lusaka miongoni mwa viongozi wengine.