Serikali imetangaza mabadiliko kadhaa yanayolenga kuboresha huduma kwa abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA.
Mpango huo unaohusisha serikali yote unalenga kuhakikisha huduma za ufanisi na za heshima kwa wote wanaotua na kuondoka Kenya.
Serikali imetambua haja ya kulainisha mifumo ya kuingia nchini kwa lengo la kupunguza muda wa kusubiri na kupunguzia abiria usumbufu.
Kwa kufanya hivyo maafisa katika uwanja wa JKIA wataimarisha sifa za Kenya kama eneo linalokaribisha wote huku wakihakikisha uzingatiaji wa mipango yote inayohitajika.
Sambamba na mitindo bora ya kimataifa, serikali ya Kenya itatoa kipaumbele kwa ujumuishaji wa suluhu za kiteknolojia ili kulainisha mifumo ya forodha na uhamiaji.
Juhudi zinaendelea za kuweka katika mifumo ya kidijitali stakabadhi wanazohitajika kuwa nazo wasafiri ili kuharakisha uaandaaji, kufanya usafiri kuwa bora kwa wasafiri wa ndani kwa ndani na hata wa kimataifa.
Ulinzi na faraja ya wasafiri pia vitatiliwa maanani katika uwanja huo hasa katika maeneo ambayo sio wazi kwa wote kama maeneo ya kusubiri kwa watu mashuhuri.
Ni wahudumu walio na idhini pekee watakubaliwa kufika kwenye maeneo kama hayo ndani ya JKIA hatua inayoimarisha uadilifu na usalama.
Mafisa katika JKIA watakuwa wakipokea mafunzo kila mara kuhusu huduma kwa wateja ili kuhakikisha wanaonyesha utaalamu wa hali ya juu na huduma.
Taarifa kuhusu mabadiliko hayo ilitiwa saini na waziri wa fedha John Mbadi, waziri wa barabara na usafiri Davis Chirchir, waziri wa utalii Rebecca Miano na katibu wa usalama wa taifa Raymond Omollo.