Serikali kuanzia wiki ijayo, itaanza kuyalipa madeni inayodaiwa na wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, ambao husambaza maziwa yao kwa kampuni ya New KCC.
Akiongea katika eneo la Manyatta, kaunti ya Embu, naibu rais Rigathi Gachagua, alisema serikali inatafuta masoko ya maziwa katika nchi za kigeni.
“Nitazungumza na waziri wa ustawi wa vyama vya ushirika pamoja na kampuni ya maziwa ya New KCC, kulipa madeni kufikia wiki ijayo kwa sababu ni lazima tuwapige jeki wakulima,” alisema naibu huyo wa Rais.
Naibu rais alisema mpango wa uuzaji nje maziwa pamoja na kuimarishwa kwa kampuni ya KCC hadi viwango vya kisasa , ni mojawapo ya mipango ya ajenda ya serikali ya Bottom-Up, ili kuimarisha biashara ndogo-ndogo na ukuaji wa uchumi katika maeneo ya mashinani.
Naibu rais alikuwa akihudhuria maonyesho ya mifugo pamoja na samaki katika kaunti ya Embu, yalioandaliwa na bodi ya maziwa nchini mjini Embu.
Gachagua alitangaza kwamba kuanzia mwezi huu, wakulima watapata shilingi hamsini kwa kila lita ya maziwa yanayopelekwa kwenye kampuni ya New KCC, alivyoahidiwa na rais William Ruto.
Takwimu kutoka bodi ya maziwa nchini, zinaonyesha kwamba wakulima humu nchini kwa wakati huu wanazalisha lita bilioni 5.2 ya maziwa kila mwaka.
“Kufuatia uwekezaji wa zaidi ya shilingi biliopni tano ili kuimarisha kampuni ya New KCC, shilingi hamsini ni mwanzo tu huku tukilenga kuwapatia wakulima wetu hata zaidi,” alidokeza Gachagua.