Raila: Sijaondoka katika siasa za Kenya

Tom Mathinji
1 Min Read
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Kiongozi wa muungano wa Azimio la umoja , Raila Odinga, amesema azma yake ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika haifai kueleweka vibaya kana kwamba anajiondoa kwenye siasa.

Raila alisema hata ikiwa atachaguliwa kuhudumu kwenye wadhfa huo, bado atapatikana. Raila alikuwa akiongea katika shule ya msingi ya Bar Kalare kwenye eneo bunge la Gem, wakati wa siku ya kilimo ya mwaka huu katika kaunti ya Siaya.

Raila aliahidi kuwahudumia Wa-Kenya na bara hili kwa jumla, ikiwa atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika.

Aliwaonya wale wanaodai kumpangia maisha yake ya kisiasa, akisema amekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu kuelewa muelekeo atakaohuchukua.

Wakati huo huo Raila pia alitoa wito kwa serikali kutoa fedha za kaunti ili kurahisisha utoaji huduma.

Alizihimiza serikali za kaunti kuwekeza kwenye ustawi wa kilimo na kuwaimarisha wakulima, ili waweze kuzalisha chakula cha kutosha.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliwatahadharisha wabunge dhidi ya kutumiwa na afisi ya rais kuhujumu ugatuzi, akisema wanafaa kupitisha sheria zinazoweza kuimarisha ugatuzi

Share This Article