Serikali imekariri kujitolea kulinda haki na maslahi ya Wakenya walio ugaibuni, kwa kujumuisha juhudi zao kwenye taratibu za ujenzi wa taifa.
Akizungumza alipowaaga walimu ambao wamepata ajira ya kufundisha nchini Marekani, Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi aliwahimiza walimu kuinua ubora wa elimu humu nchini ili kufikia kiwango cha kimataifa.
“Leo tunawaaga walimu ambao wamepata ajira ya kufundisha katika maneo mbalimbali nchini Marekani,” alisema Mudavadi.
“Nawahimiza walimu hawa kuinua ubora wa elimu wa taifa hili kufikia kiwango cha kimataifa na kuwa mfano bora kwa wale wanaotaka kufanya kazi ughaibuni, sio tu katika sekta ya elimu pekee, lakini pia katika tasnia zingine.”
Mudavadi alisema hatua hiyo ni ishara ya kujitolea kwa serikali kuunga mkono maendeleo ya utaalam na kufanikisha uhamishaji wa ujuzi katika soko la kimataifa.