Serikali inalenga kupanda miche ya miti bilioni moja leo Ijumaa Mei 10, 2024, siku ambayo imetengwa kwa upanzi wa miti kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na mafuriko hapa nchini.
Waziri wa mazingira mabadiliko ya tabianchi na misitu Soipan Tuya, ametoa wito kwa kila mkenya kupanda angalau miche 50, huku kila mtoto akitakiwa kupanda miche 10, ili kuhakikisha taifa linaafikia lengo la upanzi wa miche bilioni moja.
“Wananchi wanahimizwa kuhakikisha wanapiga picha miti iliyopandwa na kupachika katika mtandao wa Jaza Miti,” alisema waziri Tuya.
Mawaziri wamejukumiwa kushirikisha taasisi na idara zilizo chini yao, katika zoezi la upanzi wa miti.
Kulingana na waziri Tuya, mawaziri watatenga siku moja kila mwezi ili kushiriki katika zoezi la upanzi wa miti.
Aidha waziri huyo alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika upanzi huo wa miti, huku taifa hili likijitahidi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Natoa wito kwa wakenya kujitokeza kwa wingi kwa zoezi la upanzi wa miti katika maeneo wanakoishi na katika maeneo yaliyotengewa shughuli hiyo,” alisema waziri Tuya.
Siku hii ya upanzi wa miti imetengwa, huku serikali ikuchukua fursa ya mvua kubwa inayoendelea.