Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Pokot Kusini David Boen, ameagiza kusimamishwa kwa uchimbaji haramu wa dhahabu katika eneo la Marang’ar.
Akizungumza alipozuru maeneo ya uchimbaji madini katika eneo hilo, Boen alielezea wasiwasi wake kutokana na wachimbaji hao kutozingatia athari za mazingira na madhara yanayoweza kusababishwa kwa binadamu na wanyama.
Alisema wachimbaji madini katika eneo hilo wanahatarisha maisha yao kwa kutafuta gramu chache za dhahabu.
“Wakati wa ziara yetu, tumegundua kwamba wachimbaji dhahabu hawazingatii madhara ya kimazingira. Mwaka jana tulimpoteza mtu mmoja alipozikwa akiwa hai na mchanga, kutokana na uchimbaji haramu wa dhahabu,” alisema Boen.
Aliamuru wakazi kusitisha uchimbaji zaidi wa madini katika eneo hilo hadi wapate kibali kutoka kwa mamlaka husika za serikali.
Aidha, alisisitiza kuwa ongezeko la wachimbaji madini katika eneo hilo limeathiri sana usafi wa mazingira na usafi kutokana na ukosefu wa vyoo na hivyo kusababisha mlipuko wa kipindupindu.