Serikali imeahirisha tarehe ya kufunguliwa kwa shule hadi siku ya Jumatatu tarehe sita mwezi Mei.
Kulingana na kalenda ya elimu, tarehe ya kufunguliwa kwa shule muhula wa pili, ilikuwa leo Aprili, 29,2024.
Kwenye kwa taarifa katika mtandao wa X, waziri wa elimu Ezekiel Machogu alisema baadhi ya shule zimeathirika pakubwa na mafuriko,hali ambayo alisema huenda ikahatarisha maisha ya wanafunzi na walimu katika shule hizo.
“Ripoti ambazo wizara ya elimu imepokea kutoka kwa asasi mbali mbali za serikali, zinaashiria kuwa shule nyingi katika maeneo tofauti hapa nchini, zimeathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa. Kwa msingi huu wizara ya elimu imeahirisha ufunguzi wa shule za msingi na upili kwa wiki moja hadi Jumatatu 6, Mei, 2024,” ilisema wizara ya elimu.
Waziri alisema wizara yake itashirikiana na wadau wote katika kuchukua hatua za kukabili athari za mvua kubwa inayonyesha kwa sasa.
Hayo yanajiri huku idara ya utabiri wa hali ya anga ikionya kuwa mvua kubwa itaendelea kushuhudiwa nchini katika siku chache zijazo, huku zaidi ya watu 90 wakiripotiwa kufariki na wengine kujeruhiwa au kutoweka.