Kamati ya bunge la Seneti kuhusu uwekezaji wa umma na hazina maalum inataka tume ya maadili na kupambana na ufisadi, EACC kuchunguza madai ya ubadhirifu wa fedha za umma katika kaunti ya Kitui.
Haya yanajiri baada ya kaunti hiyo kuwekeza zaidi ya shillingi millioni moja katika kampuni ya maji na usafi ya Kitui (KITWASCO) licha ya kampuni hiyo kufilisika.
Kamati hiyo ya Seneti iligundua kuwa kampuni hiyo ilipokea kati ya shillingi millioni 8 na 10 kila mwezi kutoka kwa serikali ya kaunti na bado ina deni la shillingi milioni 500.
Umiliki wa kampuni hiyo unadaiwa kuwa wa kibinafsi licha ya kuwa ya uwekezaji wa umma wa kaunti.
Gavana wa kaunti ya Kitui Dkt. Julius Malombe Jumanne wiki hii alifika mbele ya kamati ya Seneti kujibu ubadhirifu uliofichuliwa katika ripoti ya mkaguzi mkuu wa matumizi ya fedha za umma.
Kamati hiyo kwa sasa inahoji magavana kuhusiana na kampuni za maji na usafi katika kaunti zao.