Bunge la Kitaifa na lile la Seneti yameafikiana kuhusu mabadiliko yanayopaswa kufanyiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.
Hatua hii ni afueni kwa tume hiyo ambayo kwa sasa haina makamishna wanaohitajika kuendesha shughuli zake kikatiba.
Wabunge jana Alhamisi walipitihsa sheria ya IEBC na kumaliza tandabelua ambayo imeilemaza IEBC kiasi cha kutoweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Wafula Chebukati aliyehudumu kama mwenyekiti wa IEBC na makamishna wawili Boya Molu na Prof. Abdi Guliye walistaafu mwezi Januari mwaka jana.
Makamishna wengine wanne wakiongozwa na Juliana Cherera walitimuliwa na Rais William Ruto kwa kupinga matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Tayari eneo bunge la Banissa, kaunti ya Mandera na wadi mbili eneo la Magharibi ya Kenya, hayana wawakilishi kutokana na kutoandaa uchaguzi mdogo.
Sheria hiyo inayosubiri sahihi ya Rais inapendekeza kubuniwa kwa jopo la watu tisa watakaowateua makamishna wa tume hiyo.
Bunge la Seneti lilikubaliana na kupitisha mapendekezo kuhusu IEBC huku Bunge la Kitaifa likiafikiana jana Alhamisi.
 
					 
			 
                                
                              
		 
		 
		 
		