Serikali ya Senegal imeamua kusimamisha safari za nje ambazo si za lazima kwa mawaziri na maafisa waandamizi, ikionya kuwa kipindi kijacho kitakuwa kigumu kiuchumi.
Hatua hiyo imechochewa na mvutano unaoendelea kati ya Marekani, Israel na Iran ambao umechangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani na kuongeza mzigo kwa bajeti ya nchi.
Pamoja na hali ya vita, kufungwa kwa njia muhimu ya Bahari ya Hormuz kumevuruga usambazaji wa nishati kimataifa. Matokeo yake ni kupanda kwa bei ya mafuta ghafi ya Brent, hali inayozisukuma serikali nyingi kuchukua hatua za kupunguza madhara ya ongezeko hilo kwa wananchi na uchumi wao.
Akizungumza na vijana katika mji wa pwani wa Mbour Ijumaa jioni, Waziri Mkuu Ousmane Sonko alisema bei ya mafuta sasa iko karibu dola 115 kwa pipa, kiwango kilicho juu zaidi ukilinganisha na makadirio ya bajeti ya dola 62.
Alisisitiza kuwa safari za nje zitaruhusiwa tu pale zinapokuwa za lazima, akiongeza kuwa tayari amefuta ziara zake zilizopangwa kwenda Niger, Hispania na Ufaransa.
Katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo, nchi mbalimbali za Afrika Magharibi na kwingineko zimeanza kuchukua hatua kama kuongeza bei ya mafuta, kutoa ruzuku na kuhimiza kazi kufanyika kwa njia ya mtandao.
Sonko alieleza kuwa Senegal, ambayo tayari inakabiliwa na deni kubwa, italazimika kufuata mkondo huo, huku akiahidi kuwa hatua zaidi zitatangazwa wiki ijayo na Waziri wa Nishati na Madini atatoa ufafanuzi wa kina hivi karibuni.