Selena Gomez ajibu wakosoaji wake

Marion Bosire
1 Min Read

Mwimbaji wa Marekani Selena Gomez ambaye pia ni mwigizaji na mfanyabiashara ametetea mwonekano wake.

Gomez wa umri wa miaka 32 alikuwa akijibu wakosoaji wake mitandaoni waliotoa maoni kuhusu mwonekano wake wa unene wakati wa uzinduzi wa filamu “Emilia Perez”.

Alielezea kwamba ana tatizo fulani kwenye utumbo ambalo humfanya aonekane mnene akiongeza, “Sijali kwamba sionekani mwembamba. Sina mwili huo. Mwisho wa simulizi!”

Yeye na wenzake walipigwa picha nje ya ukumbi wa filamu wa DGA Jumanne wakati wa uzinduzi wa filamu yake ambapo anaigiza kama Jessi.

Tatizo alilotaja Gomez ni la”small intestinal bacterial overgrowth” almaarufu SIBO linalosababishwa na ukuaji kupita kiasi wa bakteria kwenye utumbo mdogo.

Nyota huyo alielezea kwa hasira kwamba tatizo hilo hupungua na kuongezeka kila mara na hivyo kuathiri pia uzani wa mwili ikizingatiwa kwamba ana matatizo mengine ya kiafya.

Julai 2024, Gomez alilazimika pia kuzima minong’ono mitandaoni pale alipojibu baada ya video kusambazwa ikimwonyesha kwenye afisi ya mpasuaji wa urembo huko Florida.

Wakati huo Gomez alisema alighadhabishwa na shuku shuku za watu kwamba alikuwa amefanyiwa upasuaji wa kuboresha mwonekano wake.

Alifafanua kwamba uboreshaji aliofanyiwa ni wa uso pekee huku akitaka wanamitandao waachane naye.

Share This Article