Idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema baadhi ya maeneo ya nchi yatashuhudia kipindi cha ukavu na jua huku mvua kubwa ikiendelea nchini.
Kwenye utabiri wa hivi punde, idara hiyo imesema viwango vya joto vya zaidi ya nyuzi 30 vinatarajiwa katika maeneo ya Pwani, Kaskazini Mashariki, Kaskazini Magharibi na Kusini mwa Nyanza.
Utabiri huo ni wa kipindi cha wiki moja kuanzia leo hadi Disemba 4.
Utabiri huo unaonesha kuwepo kwa mvua katika nyanda za chini kusini mwa nchi ambako sehemu nyingi zitapokea mvua ya hadi mililita 50.
Mnamo siku ya Jumapili, halmashauri ya maji ilitoa tahadhari ya mafuriko ikisema watu wanaoishi katika sehemu ambazo hukumbwa na mafuriko, wanapaswa kujiandaa kwa uwezekano wa kutokea kwa mafuriko kutokana na ongezeko la mvua kubwa.
Afisa mkuu mtendaji wa halmashauri hiyo Reuben Ngessa alisema hali hiyo itashuhudiwa hadi wiki ya kwanza ya mwezi Disemba.
Aidha, aliwaonya waepukane na kuzuru sehemu ziliko mito na sehemu zingine zilizofurika kwa miguu au kwa kutumia gari.